Maana ya Ndoa

Maana ya ndoa

Ndoa ni muunganiko kati ya mwanamume na mwanamke, walio amua kwa ridhaa yao wenyewe kuishi pamoja kama mke na mume mpaka mwisho wa maisha yao ya ndoa.

Aina za ndoa kwa mujibu wa sheria

Kuna aina mbili tu za ndoa zinazotambulika na sheria ya ndoa Tanzania

 • Ndoa ya mke mmoja na mume mmoja tu.
 • Ndoa ya wake wengi.

Ndoa hizo zinaweza kusheherekewa kufuatana na misingi na taratibu za kidini, kimila au kiserekali, kushuhudiwa na watu wasiopungua wawili na kusajiliwa kwa mujibu wa sheria.

Hatua za kuchukua kabla ya ndoa kufungwa

 • Lazima taarifa ya nia ya kufunga ndoa itolewe siku 21 kabla ya ndoa kufungwa, kama kutakuwa na mwenye pingamizi budi litolewe itoe kabla ya ndoa kufungwa
 • Majina ya wale wanaotarajia kufunga ndoa, umri, majina ya wazazi wao na mahali wanapoishi yatajwe.
 • Tamko kwamba wanaotarajia kufunga ndoa hawana uhusiano unaokatazwa kisheria kufunga ndoa

KUSAJILI NDOA

Ndoa inaweza kufungwa Kiserikali au kwa madhehebu ya Kikristo au Kiislam au kufuatana na mila na desturi za wale wanaofunga ndoa.

Msajili wa ndoa atatoa cheti cha ndoa. Kila Ndoa inapofungwa lazima iwe na mashahidi wawili

Mambo ambayo sheria ya ndoa inakataza katika suala zima la kuoa au kuolewa

 • Mwanamke na au mwanaume kuolewa/kuoa bila ridhaa yake mwenyewe
 • Mwanamke na mwanaume wenye undugu wa damu kuoana
 • Mwanamke na mwanaume kuoana kabla ya kutimiza umri unaoruhusiwa kisheria (kwa mwanaume miaka 18 na kwa mwanamke miaka 18 au 15 kwa idhini ya wazazi/mlezi wake)
 • Kuoana watu wa jinsia moja
 • Mwanamke na mwanaume kutaka kuoana kwa mkataba wa kipindi maalum.

Haki za mume na mke katika ndoa

 • Wote wana haki ya kumiliki mali kama nyumba, shamba n.k. kwa majina yao binafsi;
 • Wote wana haki ya kutoa idhini katika uuzaji au kwa pamoja kuweka dhamana mali yoyote ya familia;
 • Wote wana haki ya kuishi katika nyumba ya familia iwapo mume/mke amemkimbia;
 • Mke ana haki ya kupewa matunzo yake na ya watoto wakati wa ndoa au iwapo mume amemkimbia, wameachana kwa amri ya mahakama. Na mume ana haki ya kupewa matunzo iwapo ana ulemavu hawezi kujiingizia kipato kutokana na ulemavu au ugonjwa wake;
 • Wote wana haki ya kutokupigwa na au kufanyiwa ukatili wa aina yoyote;
 • Wote wana haki ya kupeana unyumba;
 • Wote wana haki ya kutumia mali ya ndoa;
 • Wote wana haki kuomba amri ya talaka.

Ukomo wa ndoa Ukomo wa ndoa uko wa aina mbili:

 • Kifo cha mwanandoa mmoja wapo
 • Talaka ambayo imetolewa na Mahakama pekee pale inapojiridhisha kwamba kuna sababu ya msingi kufanya hivyo.

Baraza la usuluhishi la Ndoa

Baraza la usuluhishi la Ndoa, ni baraza lililoanzisha na kifungu 102 cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, sura ya 29 kama sheria zilizopitiwa mwaka 2002, kwa madhumuni ya kusuluhisha wanandoa ambao wanaingia kwenye migogoro ya Ndoa. Kazi za Baraza la Usuluhishi la Ndoa:-

 • Kusuluhisha Wanandoa walioko kwenye Ndoa baada ya kupokea lalamiko toka kwa mmoja wapo wa Wanandoa
 • Kutoa hati maalum kuthibitisha kuwa suluhu imeshindikana na kuelekeza wanandoa kwenda Mahakamani kwa amri zaidi.

MUHIMU: Mahakama peke yake ndiyo ina mamlaka ya kutoa amri ya kutengana au talaka

Sababu zinazopelekea au kuishawishi mahakama kuvunja ndoa:-

 • Uzinzi kati ya wanandoa
 • Ukatili kati ya wanandoa au watoto wa ndoa
 • Dharau au kupuuza kulikokidhiri dhidi ya mwenzi
 • Kumtelekeza mwenzi kwa zaidi ya miaka mitatu Pale mwenzi anapofungwa kifungo cha maisha au kwa kipindi kisicho pungua miaka miaka mitano
 • Ikiwa mwenzi ameugua ugonjwa wa akili na imedhibitishwa na daktari kwamba hakuna uwezekano wa kupona.
 • Kubadili dini baada ya ndoa kufungwa pale wanandoa wote walikuwa wakifuata imani ya dini moja.

Haki za wanandoa zinazoambatana na amri ya talaka

 • Mgawanyo wa mali za ndoa /familia
 • Matunzo ya mke Hifadhi na matunzo ya watoto
 • Kizuizi cha kutobugudhiwa
 • Kuoa/Kuolewa tena
 • Fidia ya uzinzi
 • Gharama za kuendesha Shauri la Talaka

Haki ya Mgawanyo wa mali za familia/ ndoa Mali yoyote ambayo imepatikana wakati wa uhai wa ndoa na kwa nguvu na au machango wa pamoja wa wanandoa.

Iwapo mali iliyopatikana na mwanandoa mmoja wapo kabla ya ndoa au kwa nguvu zake mwenyewe lakini imeboresha/imetunzwa na mwanandoa mwingine mali hiyo itatambulika kama mali ya ndoa.

Lakini kama kuna mali yoyote ambayo mwanandoa mmoja amempa mwanandoa mwenzake kama zawadi, mali hiyo itakuwa ya yule aliyepewa pekee.

Aina za mchango

Kutekeleza kazi nyumbani hasa kutunza familia; mfano kuosha vyombo, kupika, kufua nguo, kubeba maji na kazi zingine zinazofanana na hizo kwa maslahi ya familia.

Kutunza mali za ndoa: mfano kufyeka, kulima, kuvuna shamba, kufanya marekebisho ya mali za ndoa kwa maslahi ya familia.

Mchango wa fedha wa mwanandoa katika kununua mali.

Haki ya Matunzo ya mwanandoa

Jukumu la kutoa matunzo kwa mke na watoto ni la mume, jukumu hilo litatekelezwa wakati wa uhai wa ndoa na baada ya talaka.

Haki ya Hifadhi na matunzo ya watoto

Hifadhi ya watoto hutolewa kwa mume au mke au mtu baki (mlezi) hasa kwa kuzingatia ustawi na maslahi ya wale watoto. Zaidi ya hayo, mahakama pia inaweza kuzingatia yafuatayo:

Umri wa wale watoto, mfano, watoto walio chini ya miaka saba kipaumbele cha hifadhi hupewa mama mzazi; labda kama kutakuwa na sababu za msingi za kuto fanya hivyo. Mfano kama mama mzazi ana matatizo ya kiakili, anaishi katika mazingira hatarishi.

Mazingira ya mahali watakapoishi watoto, mfano, kama mazingira ya upande mmoja ni hatarishi kwa ustawi wa mtoto, basi haki ya hifadhi atapewa mzazi mwingine bila kujali umri.

Matakwa ya wazazi wa mtoto nani kati yao angependa kupewa hifadhi ya watoto

Mila na desturi za jamii ambayo wanandoa wametokea.

Kama mtoto anaumri zaidi ya miaka saba na ana uelewa wa kutoa mapendekezo yake, basi matakwa/maoni yake yatasikilizwa zaidi.

Haki ya hifadhi ya mtoto haimnyimi mzazi mwenza haki ya kumuona na au kumtembelea mtoto/watoto. Haki ya hifadhi ya mtoto haiondowi jukumu la baba kutoa matunzo.

TOP